Serikali imesema hadi kufikia Mwezi, Machi 2024 jumla ya vijiji 11,837 sawa na asilimia 96.37 ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishiwa huduma ya umeme.

Hayo yamesema na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko Bungeni, Jijini Dodoma wakati akisoma Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/2025.

Aidha, Dkt. Biteko amesema katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa Wananchi vijijini, jumla ya taasisi 63,509 zinazotoa huduma kwa jamii ikiwemo ya elimu, biashara, pampu za maji, vituo vya afya na nyumba za ibada zilikuwa zimeunganishiwa umeme, ikilinganishwa na taasisi 43,925 Mwezi Aprili, 2023.

Vilevile, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kupeleka umeme vitongojini na katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa, vituo vya afya na pampu za maji, wachimbaji wadogo wa madini, viwanda na kilimo, katika shule pamoja na mahakama za mwanzo vijijini.

Dkt. Biteko amesema katika mwaka 2024/25, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kupeleka nishati vijijini ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii katika maeneo hayo. 

Miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 20,000 ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ununuzi wa wakandarasi wa kutekeleza mradi, kufanya usanifu wa kina wa mradi na kuanza ujenzi wa miundombinu ya mradi.

Miradi mingine ambayo itapewa kipaumbele ni pamoja na Mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 3,060 (vitongoji 15 kila Jimbo) kwa kujenga miundombinu ya mradi, kufunga transfoma na kuunganisha wateja.

Miradi mingine, itakayotekelezwa ni mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili (B); Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili (C); Mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya Vijijini-Miji; (PERI Urban); Mradi wa kusambaza umeme katika Migodi Midogo, Maeneo ya Kilimo na Viwanda; Mradi wa kupeleka umeme katika minara ya mawasiliano ya simu na mradi wa ufungaji wa mifumo ya umeme jua kwenye makazi yaliyopo Visiwani na yaliyopo mbali na Gridi ya Taifa.

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau, itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 – 2034 kwa kupatia ufumbuzi vikwazo vya matumizi ya nishati hiyo, ikiwemo gharama kubwa, upatikanaji hafifu na uhaba wa miundombinu yake na kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya nishati zisizo safi na salama za kupikia.

Aidha, Mradi wa kusambaza majiko banifu kwenye Kaya zilizopo katika maeneo ya Vijijini na Vijiji-Miji; kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa mkaa mbadala kwa ajili ya ununuzi wa mashine zitakazotumika katika uzalishaji wa mkaa huo; kuendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza katika ujenzi wa miundombinu ya nishati ya kupikia katika maeneo 211 pamoja na kuendelea na usambazaji wa gesi asilia majumbani, hususan katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani.

Na Mwandishi wetu

Kikao cha 23 Jukwaa la kudumu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Watu wa Asili (UNPFII) kinaendelea jijini New York nchini Marekani. Kikao hicho kinahudhuriwa na ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Prof. Hamisi M. Malebo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe wengine wa Tanzania wanaohudhuria mkutano huo ni pamoja na Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Hindu Zarooq Juma, Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Pellage Kauzeni, Afisa Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Agnes Gidna, Kaimu Meneja wa Urithi wa Dunia katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Edward Kutandikila, Mwanasheria wa Serikali na Erick J. Kajiru, Afisa Mwandamizi Mkuu katika Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ujumbe wa Tanzania umempongeza Mwenyekiti wa Kikao cha Jukwaa la 23 la Umoja wa Mataifa la Watu wa Asili Hindou Oumarou Ibrahim na Mwenyekiti mwenza kwa kuongoza vizuri kikao cha Jukwaa.

Prof. Hamisi Malebo ameueleza mkutano huo kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kusisitiza msimamo wake wa muda mrefu kwamba hakuna wananchi waliohamishwa kwa nguvu katika tarafa za Ngorongoro na Loliondo kama inavyodaiwa na madai hayo ni ya uongo. Alibainisha kuwa mashauriano na wakazi wa Ngorongoro na Loliondo yalifanyika kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto za maeneo yote mawili ya hifadhi, mtawalia.

Eneo la kilomita za mraba 4,000 katika eneo la Loliondo ambalo lilikuwa halijawahi kukaliwa na watu na lilipewa hadhi ya hifadhi mwaka 1895 na utawala wa wakoloni wa Kijerumani na limeendelea kuwa hadhi hiyo hadi lilipogawanywa.

Historia iko wazi kuwa, Waamasai na makabila mengine walianza kulivamia eneo hilo baada ya uhuru wa Tanganyika kuanzia mwaka 1961.

Kwa kuzingatia haki za binadamu na maisha ya wananchi waliovamia eneo la Loliondo, Serikali ilitenga eneo la kilometa za mraba 2,500 kwa ajili ya wananchi na kilometa za mraba 1,500 kubakizwa kwa ajili ya uhifadhi wake na kuitwa Pori la Akiba la Pololeti.

Prof. Malebo ameihimiza Sekretarieti ya Jukwaa la Masuala ya Watu wa Asili la Umoja wa Mataifa kutambua na kufahamu ukubwa wa kilometa za mraba 2,500 ulivyo pamoja na mpango mahsusi wa Serikali wa kuweka uwiano wa utekelezaji wa haki za binadamu, uhifadhi na maendeleo ya wananchi.

Prof. Malebo akiwakilisha katika mkutano huo, alieleza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasikitishwa na utaratibu wa kuandaa mapendekezo ya Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ambapo mara nyingi maelezo ya Nchi Wanachama hayazingatiwi na huwa ya upande mmoja na hayana uwiano.

Alibainisha kuwa Mataifa Wanachama kama nchi ya Tanzania wameshiriki katika kongamano hili kwa nia njema na kutoa upande wa pili wa maelezo ambao tunaamini unasaidia jukwaa kupata uelewa wa kutosha wa masuala yanayowasilishwa katika mkutano.

Alieleza tabia ya kuchagua na kupendelea katika kuandaa taarifa za mkutano ni hatari na inaleta migawanyiko.

Alitoa wito kwa kongamano kutumia njia ya kutopendelea na yenye uwiano sawa ili kuakisi mada na taarifa zinazowasilishwa katika Mkutano huo.

Ujumbe wa Tanzania umebainisha kuwa Mwandishi wa Kudumu wa Haki za Watu wa Kiasili atakuwa akizuru Tanzania ili kuthibitisha madai kuhusu Ngorongoro na Loliondo, hivyo umelishauri Jukwaa kuwa ni mapema sana kutoa mapendekezo kuhusu Tanzania kabla ya Mwandishi kuwasilisha taarifa ya ziara yake.

Prof. Malebo ameuhakikishia mkutano huo kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaongozwa na utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Kwa hali hiyo, imezingatia haki za binadamu kwa wananchi wake wake wakati ikishughulikia changamoto katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo na Hifadhi ya Ngorongoro.

Na Mwandishi Wetu, Arusha

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), imetoa mafunzo maalumu kwa akina mama lishe 50 wa mkoa wa Arusha kwa lengo la kuwaelimisha namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali ya moto.

Mbali na mafunzo hayo, pia GGML imewagawia mitungi 50 ya gesi ya kupikia kwa ajili ya kuhamasisha akina mama hao kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kisha kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.

Mafunzo hayo yalitolewa jana katika maadhimisho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika Kitaifa Jijini Arusha kuanzia tarehe Aprili 23 hadi Mei Mosi 2024.

Akizungumza na akina mama lishe hao, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira kutoka GGML, Dk Kiva Mvungi amesema wamemua kutoa elimu kwa akina mama hao ili watambue namna ya kupambana na moto majumbani na kuzingatia usalama kwenye maeneo yao ya biashara hasa ikizingatiwa wao ni chanzo kikubwa cha kukutana na watu wengi.

“Tunawafundisha namna ya kupambana na majanga ya moto kwani shughuli zao za kila siku zinahusiana na masuala ya moto na matumizi ya mkaa na gesi.

“Lakini pia ni vema kutambua namna gani mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri watu pia namna tabia zetu binafsi zinavyoweza kuchangia kuachana na ukataji hovyo wa miti,” amesema.

Amesema athari za mabadiliko ya tabia nchi, zinamuathiri kila mmoja bila kujali, cheo, mkubwa au mdogo hivyo ni vema kila mmoja kuzingatia matumizi ya nishati safi ili kuondokana na majanga yatokanayo na mabadiliko hayo.

“Tumeandaa elimu hii kuona namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa sababu ukataji wa miti ukikithiri unasababisha mmonyoko wa ardhi, mafuriko na ongezeko la joto duniani.

“Matumizi ya mkaa au kuharibu vyanzo mbalimbali ambavyo vinaweza kusabababisha athari kwenye mazingira na kusababisha mafuriko hata kwenye maeneo yetu ya uchimbaji,” amesema.

Kwa upande wa Ofisa Mwandamizi wa masuala ya jamii na maendeleo ya kiuchumi kutoka GGML, Ruth Mharagi amesema katika mafunzo hayo, wamewafundisha akina mama hao namna salama ya kutumia nishati ya gesi na kuwasisitiza kuondokana na matumizi ya mkaa.

“Lakini pia kwenye banda letu tumeendelea kupokea wageni wanaopenda kujifunza namna ya kupambana na majanga ya moto kwa sababu asilimia kubwa wanauelewa mdogo namna ya kukabiliana na majanga ya moto majumbani,” amesema na kuongeza;

“Watu wengi hawajui njia za awali za kupata msaada wa kuzima moto, sisi tunatoa mafunzo hayo, kuna vifaa vya kawaida ambavyo mama yeyote anavyo nyumbani, mfano ndoo ya maji, taulo, kanga au kitenge vilivyolowekwa kwenye maji, ni vifaa vya kawaida ambavyo unaweza kutumia kuzima moto hivyo tunaendelea kuwaribisha kwenye mabanda yetu,” alisema.

Wakati huo huo Mkaguzi wa afya ya mazingira ya kazi kutoka OSHA, Elizabeth Mtile amewasisitiza akina mama hao kuzingatia umuhimu wa kufuata sheria na miongozo mbalimbali ya usalama na afya katika maeneo ya kazi.

“Kauli mbiu yetu inayosema athari za mabadiliko ya tabia nchi katika usalama na afya kazini, inalenga kudhibiti majanga na mabadiliko haya ya tabia nchi kwa kushirikisha kila kundi kwenye jamii kwani athari hizi zinatugusa sisi sote,” amesema.

Mmoja wa akina mama lishe hao, Prinsila Kwai aliishukuru GGML na OSHA kwa kupatia mafunzo hayo kwani yanaenda kuwa chachu ya mabadiliko kwao na kwa wale wanaowazunguka.

“Kwa kweli tunashukuru sana kwa shughuli zetu za kila siku zinahusiana na moto hivyo mafunzo haya yatatusaidia sana namna ya kukabiliana na mlipuko labda wa gesi,” amesema.
 

Mratibu wa idara ya dharura (ERT) kutoka GGML, Mohamed Mwaimu akimuonesha mama lishe namna ya kuzima moto wakati inatopokea mtungi wa gesi unapopata hitilafu na kulipuka. Mafunzo hayo yametolewana GGML kwa kushirikiana na OSHA kwa akina mama lishe 50 wa mkoani Arusha.
 

Ofisa Mwandamizi wa masuala ya jamii na maendeleo ya kiuchumi kutoka GGML, Ruth Mharagi akimgawia mtungi wa gesi ya kupikia mmoja wa akina mama lishe waliopatiwa mafunzo ya namna ya kuzima majanga ya moto wakati wanapoendelea na shughuli zao za kupika. Mafunzo hayo yametolewana GGML kwa kushirikiana na OSHA kwa akina mama lishe 50 wa mkoani Arusha ambao pia wote waligawiwa mitungi ya gesi.
 

Mratibu wa idara ya dharura (ERT) kutoka GGML, Mohamed Mwaimu akiwaonesha mama lishe namna ya kuzima moto wakati inatopokea mtungi wa gesi unapopata hitilafu na kulipuka. Mafunzo hayo yametolewana GGML kwa kushirikiana na OSHA kwa akina mama lishe 50 wa mkoani Arusha.
 

Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira kutoka GGML, Dk. Kiva Mvungi (kulia) akizungumza na akina  mama lishe kuwaeleza namna ya kuzima moto wakati inatopokea mtungi wa gesi unapopata hitilafu na kulipuka. Mafunzo hayo yametolewana GGML kwa kushirikiana na OSHA kwa akina mama lishe 50 wa mkoani Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati Wimbo wa Taifa wa Tanzania na ule wa Afrika Mashariki ukiimbwa katika Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi mara baada ya kushuka kwenye gari Maalum la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Aprili, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Aprili, 2024.
Benki ya CRDB kupitia sera yake ya uwekezaji kwa jamii, Aprili 24 - 25, 2024 ilikabidhi madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Kikilo na madarasa mengine mawili katika Shule ya Msingi Isabe zote za wilayani Kondoa, mkoa wa Dodoma yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki hiyo.

Hafla ya kukabidhi madarasa hayo, iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi ambaye aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa pamoja na Maafisa Elimu Sekondari na Msingi.

Katika hafla zote mbili Dkt. Khamis Mkanachi ameishukuru Benki ya CRDB kwa kukubali maombi ya ujenzi wa madarasa katika Wilaya ya Kondoa, ambayo yapo katika vijiji vya Kikilo na Bukulu. Huku akitoa rai kwa wanafunzi kusoma kwa bidii kwani mazingira ya shule yanaendelea kuboreshwa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa, Mashauri Vicent aliyekabidhiwa madarasa hayo ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya elimu pia kuahidi kuwa watahakikisha madarasa hayo yanakuwa ni sehemu ya kuchagiza ongezeko la wanufaika ambayo ni watoto kwenye jamii ya Kondoa.

Kwa upande wa Benki ya CRDB, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay aliyeongozana na Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji kwa Jamii pamoja na Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati, amesema kuwa Benki ya CRDB imeweka sera ya uwekezaji kwa jamii inayolenga kuchangia maendeleo mbalimbali katika jamii hasa katika swala la Elimu, Mazingira, Afya, Vijana na Wanawake. Aidha, ametoa rai kwa wazazi wa shule hizo kuendelea kushirikiana kwa karibu na uongozi wa shule katika kuboresha miundombinu ya shule.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay wakiwa pamoja na viongozi wengine pamoja na Wanafunzi katika moja ya madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 katika Shule ya Msingi Isabe, iliyopo katika kijiji cha Bukuru, Wilayani Kondoa, katika hafla  iliyofanyika Aprili 25, 202.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi (wanne kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay muda mfupi baada ya kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay (katikati) akiwa pamoja na viongozi wengine wa Benki ya CRDB pamoja na wa Halmashauri ya Kondoa wakiwa katika picha ya paamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kikilo, muda mfupi baada ya kukaidhi madarasa mawili katika shule hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi akizungumza wakati wa hafla kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay akizungumza wakati wa hafla kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.












Na WAF, TABORA

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameziasa Kamati za Ulinzi na Usalama nchini kuona umuhimu wakuifanya ajenda yakutokomeza Malaria iwe yakudumu kwenye vikao vya maamuzi.

Dkt. Mollel ameyasema hayo leo, Aprili 25, 2024 akiwa amemwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye kilele cha Siku ya Malaria Duniani iliyofanyika mkoani Tabora na kusema kuwa kama nchi imeendelea kupiga hatua katika vita hivyo ikilinganishwa na miaka zaidi ya ishini iliyopita ambapo maambuki na vifo vya Malaria vilikuwa kati ya asilimia 45 hadi 50.

Aidha Dkt. Mollel amesema azma ya Serikali ni kufikia asilimia 3.5 ifikapo 2025 na kuwa na ziro Malaria 2030 huku akisisitiza kwa kusema itafikiwa endapo juhudi za Makusudi zitafanywa kwa ushirikiano baina ya Serikali na wadau

"Leo tunazungumza asilimia 8.1 kama nchi lakini miaka ya 1998, tulikuwa na kiwango cha juu sana, hivyo ili tuweze kufikia adhma yakumaliza kabisa malaria ifikapo 2030 kila mmoja wetu anawajibu wakufanya" amesema Mollel.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI Samsoni Maella, amesema Utumiaji wa Mifumo ya GoTHOMIS na FFARS imekuwa chachu ya kukusanya takwimu sahihi kwa ajili ya ngazi ya maamuzi, hali iliyochangia kufanya maamuzi sahihi kutokana na kuwa na takwimu sahihi.

"Kama Ofisi ya Rais TAMISEMI, tumefanikiwa kuimarisha miundo mbinu ya Afya na Rasilimali watu mathalani miaka mitatu nyuma tulikuwa na Hospitali za Wilaya 77 leo hii tunazo 177 hizi zimechochea sana uimarishaji wa huduma” amesema Mahela.

Naye Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI Dkt. Hamis Kigwangala ametoa wito kwa serikali na wadau kuongeza afua za kutibu watoto Shuleni, pia wafike maeneo ya Migodi, Mashamba Makubwa na maeneo ya Wafugaji.

Awali Msimamizi wa Miradi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim, akiwa amemwakilisha Katibu Mkuu, amesema kuchaguliwa kwa mkoa wa Tabora kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Wiki ya Malaria, ni pamoja na kuongeza nguvu ya afua za kupambana na Malaria kutokana na Mkoa huo kuwa na Maambukizi ya juu ya Ugonjwa huo ya asilimia 23.4 kwa sasa kutoka asilimia 11.7 kwa mwaka 2011.






Mkutano Maalum wa 53 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika leo tarehe 25 Aprili 2024 Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Mkutano huo, pamoja na masuala mengine umejadili na kupitisha Makadrio ya Bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb.).

Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Naibu Waziri Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb.) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi

Mkutano huo umefanyika kufuatia kukamilika kwa kikao cha ngazi ya Makatibu Wakuu kilichofanyika tarehe 24 Aprili 2024 ambacho kilitanguliwa na kikao cha ngazi ya Wataalam cha tarehe 23 Aprili 2024.








Top News